
Marehemu Levina Mmasi akilishwa
chakula na aliyetarajia kumuoa, Kasisi Masawe kwenye hafla ya kuagwa
kwake (Send-Off Party) iliyofanyika Jumatano iliyopita.
Handeni. Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Bibi Harusi ambaye
ni mkazi wa Chanika mjini Handeni, Levina Mmasi (23) amefariki dunia
saa moja kabla ya ndoa yake kufungwa katika Kanisa la Katoliki la Roma
Wilaya Handeni Jumamosi na hivyo kuilazimu kamati ya maandalizi ya
harusi kujigeuza na kuwa ya msiba.Kifo hicho kilichotokea Jumamosi mwishoni mwa wiki iliyopita,
kimekuwa gumzo mjini Handeni huku wananchi wakisema kuwa ni tukio
ambalo halijawahi kutokea katika wilaya hiyo.
Msemaji wa familia ya marehemu aliyejitambulisha kwa jina la
Firmin Mrimasha, alisema kuwa chanzo cha kifo cha Levina ambaye
alijifungua mwanzoni mwa wiki iliyopita,ilikuwa ni homa aliyoipata
ghafla siku ya Alhamisi na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya
Handeni na kukutwa na malaria na kisha kulazwa kwa matibu.
“Huyu bibi harusi alikuwa ametoka kujifungua, alikuwa na
mtoto wa kiume kutokana na ujauzito wa miezi saba, ndipo ghafla Alhamisi
akapata homa tukampeleka hospitali alikolazwa na baada ya kupata nafuu,
aliruhusiwa Ijumaa.
“Baada ya kuruhusiwa akaanza maandalizi ya harusi na Jumamosi
ambayo ndiyo siku ya ndoa yake, alijiandaa lakini ilipofika saa 8.05
akafariki dunia akiwa nyumbani akisubiriwa kwenda kanisani kufunga ndoa
ambayo ilikuwa ifungwe saa 9.00,” alisema Mrimasha.
Alisema, “Inasikitisha sana ila imeshatokea yaani marehemu
amefariki saa moja kabla ya ndoa yake na baada ya kifo hicho, mtoto wake
naye alifariki muda mfupi baada ya mama yake kufariki dunia,” alisema
Mrimasha.
Akizungumzia mkasa huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Harusi hiyo
iliyogharimu Sh7.7 milioni, Abdi Kipacha alisema kuwa kwake ni tukio la
kwanza kutokea tangu kuzaliwa kwake na kamwe hawezi kulisahau.
“Nilishazipangia kazi kamati za maandalizi, lakini ghafla
tukapewa taarifa kuwa bibi harusi amefariki…Hatukuamini, ikabidi
niwatangazie wanakamati wenzangu kuwa hakuna tena shughuli, bibi harusi
amefariki,” alisema mwenyekiti huyo wa kamati na kuongeza:
“Kitu tulichokuwa tukisubiri ni kuambiwa bibi harusi angefika
saa ngapi, lakini ghafla tukapewa taarifa za kifo, ilikuwa ni vigumu
kuamini lakini ni kweli imetokea na inasikitisha kwani si jambo la
kawaida,” alisema Kipacha.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na wanandugu ni kuwa
marehemu alikuwa Mwalimu wa Shule ya Msingi Nndawa mkoani Lindi na
kwamba alikuwa katika kundi la walimu wa ajira mpya ambayo hadi mauti
yanamkuta alikuwa hajapokea hata mshahara wake wa awali.
Akizungumzia hali hiyo, Padri aliyekuwa afungishe ndoa hiyo,
Max Sabuni wa kanisa hilo Katoliki Handeni alisema:
“Nimesikitishwa na tukio hili kwa kuwa halikuwahi kunitokea…Kilichobaki
ni wanandugu kuwa watulivu kwa kuwa Mungu amechukua kiumbe wake kwa muda
alioupanga.”
Aliwataka ndugu, jamaa na marafiki kuwa na subira katika kipindi hiki cha majonzi.
Source : mwananchi.
Source : mwananchi.