
TUMIA pesa kwa akili. Unajua kwa nini? Mtazame
Mike Tyson, utapata jibu. Bondia huyo bingwa wa dunia wa masumbwi ya
uzito wa juu, ameandika historia ya aina yake ya kimaisha katika kipindi
hiki cha uhai wake.
Achana na kesi ya kufungwa jela kwa madai ya
kubaka, au tukio la kumng’ata sikio mpinzani wake ulingoni, Evander
Holyfield, Tyson, bondia aliyekuwa tishio kwenye ngumi za kulipwa na
kupiga pesa za maana sasa kipato chake ni Dola 1 Milioni tu.
Wakati anang’ara ulingoni, bondia huyo alitajwa
kuwa na kipato kinachofikia Dola 300 milioni, lakini kwa sasa
anaripotiwa kubaki na Dola 1 milioni ndiyo utajiri wake aliobaki nao.
Makuzi yake
Tyson alizaliwa Juni 30, 1966 huko Brooklyn New
York, Marekani kwenye eneo hatari sana. Akiwa na umri wa miaka 13 tu,
Tyson alikuwa tayari amekamatwa na polisi mara 38 na alikuwa akifanya
matukio ya hatari sana.
Utukutu wake ulizidi zaidi alipojiunga na shule ya
wavulana ya Tryon, mahali ambako alijifunza ngumi. Bobby Stewart, ndiye
aliyeanza kumfundisha ngumi bondia huyo kabla ya kumkabidhi kwa kocha
Cus D’Amato.
Cus D’Amato aliendelea kumnoa Tyson hadi hapo
alipoanza kumsimamia kisheria kutokana na mama yake Tyson kufariki dunia
wakati huo bondia huyo akiwa na umri wa miaka 16.
Jinsi alivyopiga pesa
Pesa kwa Mike Tyson zilipatikana kutokana na
umahiri wake ulingoni. Ushindi kwenye mapambano yake ulimfanya kuwa
bondia mwenye pesa na kupata udhamini mnono. Alikuwa akilipwa hadi Dola 5
milioni kwa pambano moja.
Ushindi wake wa kwanza ulikuwa kwenye mashindano ya Olimpiki aliposhinda medali ya fedha mwaka 1982.
Machi 6, 1985, Tyson alianza kupigana ngumi za
kulipwa wakati alipopigana na Hector Mercedes. Mambo yalikuwa mazuri na
kushinda mapambano 26 kati ya 28 na hapo alijikusanyia umarufu mkubwa.
Mwaka 1985, Tyson alipata pigo baada ya kumpoteza Cus D’Amato,
mtu muhimu zaidi kwake na hapo pesa zilianza kuwa ngumu. Februari 16,
1986, Tyson kwa mara ya kwanza pambano lake lilionyeshwa kwenye
televisheni alipomtwanga Jesse Ferguson.
Kwenye umri wa miaka 20 tu, Tyson alikuwa bondia
kijana zaidi kunyakua ubingwa wa dunia, aliwachapa James Smith, Pinklon
Thomas na Tony Tucker na kutambulika kuwa bondia bora Marekani.
Jambo hilo lilimpatia pesa zaidi baada ya kuwekwa
kwenye michezo ya kompyuta mwaka 1987, ambapo video yake ya Nintendo
iliyotambulika kama ‘Mike Tyson’s Punch-Out!!!’ iliingizwa sokoni.
Jinsi alivyofilisika
Mwaka 1988, mambo yalianza kumgeuka Tyson.
Matumizi mabaya ya pesa yalichangia kufilisika kwake. Kwenye kipindi cha
ubora wake, Tyson aliingiza pesa hadi Dola 400 milioni, lakini kabla
hata ya kufikisha umri wa miaka 39, mwaka 2004, Tyson alikuwa akiishi
kwenye madeni yanayofikia Dola 38 milioni.
Enzi zake, Tyson alikuwa ameajiri wafanyakazi 200, wakiwamo walinzi binafsi, wapishi na watunza bustani.
Tyson alitumia karibu Dola 4.5 milioni kwenye
magari na pikipiki, Dola 3.4 milioni kwenye mavazi na mapambo, Dola 7.8
milioni gharama tu za mambo binafsi, Dola 125,000 malipo ya kocha kwa
mwaka, Dola 2 milioni kurekebisha bafu la mkewe wa kwanza, mwigizaji
Robin Givens, Dola 410,000 zilitumika kwenye kusherehekea kuzaliwa na
Dola 230,000 kwenye gharama za huduma ya simu kwa miaka mitatu kutoka
1995 hadi 1998. Kwenye mahojiano yake ya hivi karibuni, Tyson alikiri
kutumia hadi Dola 500 milioni katika miaka ya 1980.
Kufilisika kulimchanganya Tyson na kumwambia mkewe
wa pili, Monica Turner kabla ya kumtaliki kwamba alikuwa ameathirika
kwa Ukimwi jambo ambalo halikuwa kweli.
Alipokuwa kifungoni, Tyson alikuwa akifanya ngono
na wanawake waliokuwa wakimtembelea gerezani, akiwamo mrembo mshauri wa
masuala ya matumizi ya dawa za kulevya, ambaye alimlipa Dola 10,000 kwa
huduma hiyo. Pombe pia zilimfanya kupoteza mkoba uliokuwa na Dola 1
milioni.
credit : MWANANCHI
credit : MWANANCHI